Mahakama yamuonya Mbowe



Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe 

Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe  
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuonya mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe kwa kutohudhuria mara mbili mfululizo kesi ya jinai inayomkabili pamoja na viongozi wengine wa chama hicho.
Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ametoa onyo hilo leo Jumanne Julai 31, 2018 kumtaka kutoacha kufika mahakamani hapo, iwapo atarudia atachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufuta dhamana yake.
Pia, ameondoa katika kumbukumbu za mahakama barua zilizowasilishwa na wakili wa utetezi, Hekima Mwasipu ambazo ni nakala ya kusudio la kukata rufaa dhidi ya uamuzi uliotolewa katika maombi ya marejeo namba 126, 2018 ya Mahakama Kuu na mwenendo wa maombi hayo.
Amesema amechukua uamuzi huo hadi pale wahusika watakapoyafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Kesi hiyo itasikilizwa tena Agosti 2, 2018 ambapo washtakiwa watasomewa maelezo ya awali.
Hayo yalielezwa baada ya washtakiwa nane kupanda kizimbani huku Mbowe akikosekana.
Wakili  Mwasipu ameieleza mahakama kuwa Mbowe hayupo lakini mdhamini wake yupo huku mdhamini huyo akieleza kuwa amefanya mawasiliano na mshtakiwa huyo na kumueleza kuwa amekwama kwenye foleni.
Pia, alieleza kuwa mawakili wanaoiendesha kesi hiyo, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya wana shughuli nyingine na wameomba kesi kuahirishwa hadi Agosti 2, 2018.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi aliiomba mahakama kumuingiza Mbowe kwenye kumbukumbu zake kuwa hiyo ni mara ya pili anashindwa kuhudhuria mahakamani bila sababu za msingi.
Washtakiwa waliokuwepo mahakamani na naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar); mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche;  mbunge wa Kawe,  Halima Mdee; mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.
Wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018 jijini Dar es Salaam.

Comments