Wazabuni watishia kuacha kulisha vyuo wasipolipwa madai
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Joyce Ndalichako
Dodoma. Baadhi ya wazabuni wametishia kusitisha huduma kwa vyuo vya ualimu vya Serikali kutokana na kutolipwa madai yao.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika baadhi ya vyuo umebaini kuwa wazabuni wametoa notisi ya kusitisha kutoa huduma ya chakula kutokana na kuelemewa na madeni madukani na katika taasisi za fedha, huku wengine wakiweka rehani mali zao.
Hata hivyo, Serikali imeendelea kusema kuwa madeni hayo ni yale ya muda mrefu ambayo yanahakikiwa kabla ya kuyalipa.
Mkuu wa chuo cha ualimu aliyezungumza kwa sharti la kuhifadhiwa jina. alisema amepokea notisi ya wazabuni wanaotaka kusitisha huduma wakisema hali ya uchumi kwao si nzuri.
Alisema anashangazwa kwamba shida hiyo kuvisakama vyuo vya ualimu ambavyo viko chini ya Wizara ya Elimu, wakati wazabuni wanaolisha sekondari ambao wako chini ya Wizara ya Tamisemi, wanalipwa fedha.
Wazabuni wanasemaje?
Wazabuni wanadai fedha za tangu Januari hadi Mei, 2018.
Mmoja wa wazabuni hao, Maseke Wambura anayehudumia Chuo cha Ualimu Mbeya, alisema hali yake ni mbaya kuliko wakati mwingine, hivyo anashindwa kufanya shughuli yoyote kwa kuwa hajalipwa na Serikali.
Wambura alisema hali aliyofikia haivumiliki baada ya wenye maduka ambako alichukua bidhaa kumsumbua kila wakati wakitaka fedha.
“Kweli nina tabu sana, tena sana. Ujue kila siku nakimbia watu maana nawindwa na watu kama digidigi ili niwape chao, nami sina,” alisema Wambura.
Mzabuni huyo alisema kila wanapowafuata wakuu wa vyuo, huambiwa hawajapokea kutoka Hazina.
Mzabuni wa Chuo cha Ualimu Nachingwea, Beda Kasembe alisema tangu Desemba, 2017 hajalipwa na benki wanataka kuuza mali zake ili kufidia deni alilokopa kuendeshea shughuli hiyo.
Kasembe alisema hali imekuwa tofauti na miaka ya nyuma wakati walipokuwa wanalisha na kulipwa fedha zao kila baada ya miezi mitatu na wakati mwingine hata kabla ya kipindi hicho.
Alisema mpango wa Serikali hauko wazi kwa sasa kama ni kuhakiki madeni au hakuna fedha, badala yake inakaa kimya na kuzua hofu kwa wazabuni.
Khadija Mfala anayepeleka chakula Chuo cha Ualimu cha Bustani kilichopo Kondoa, alisema kwa hali ilipofikia hana ujanja zaidi ya kumuachia Mungu.
Alisema kuwalisha watu kwa miezi sita bila Serikali kupunguza deni hata mwezi mmoja ni hatari kubwa kwa wazabuni hata kama wangekuwa na mitaji mikubwa.
Khadija aliiomba Serikali kulitazama suala hilo kwa jicho la kipekee kwa kuwa ilivyo sasa ni kuendelea kuwaumiza Watanzania na kuwafanya kuwa maskini licha ya kuwa walikuwa na nia njema.
“Tunawasumbua sana wakuu wa vyuo. Kila wakati wamekuwa wakituzimia simu hadi tunabadili namba au kutumia simu za watu wengine,” alisema.
“Hali ni mbaya sana hakuna namna nyingine zaidi ya kusitisha huduma.”
Ni jambo dogo
Lakini Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako alisema suala hilo si jambo kubwa kwa kiwango linavyozungumzwa.
Profesa Ndalichako alimshauri mwandishi awasiliane na katibu mkuu wa wizara yake.
“Inawezekana jambo hilo, lakini naomba uwasiliane na katibu mkuu wa wizara hata kabla ya kwenda huko Hazina,” alisema.
“Inawezekana kuna mambo madogo tu lakini kwa sasa tuko vizuri.”
Katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo alithibitisha kuwepo kwa madai, lakini akasema ni ya muda mrefu na yanahakikiwa.
Dk Akwilapo alisema mtiririko wa fedha uko vizuri na hakuna mtu anayedai fedha za muda mrefu kwa kuwa Serikali inaendelea kuzitoa kama kawaida.
Alisema madeni ambayo yanadaiwa yako katika hatua za uhakiki kabla ya kulipwa.

Comments
Post a Comment