Wabunge waing’ang’ania Stamico, wataka ivunjwe



Dodoma. Mjadala wa bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2018/19 ulitawaliwa na hoja za kutaka Shirika la Taifa la Madini (Stamico) kuvunjwa kwa maelezo kuwa linazalisha hasara badala ya faida katika miradi linayopewa kuisimamia.
Wakizungumza katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo ya ShSh58.9 bilioni bungeni mjini Dodoma jana, wabunge walitoa mfano jinsi shirika hilo lilivyoshindwa kusimamia miradi mbalimbali na kwamba Serikali inashauriwa mara kwa mara kuhusu shirika hilo, lakini hakuna kinachofanyika.
Mbunge wa Manonga (CCM) Seif Gulamali alisema shirika hilo limeshindwa kusimamia rasilimali za Taifa na kutoa mfano wa mgodi wa Buhemba ambao ulikabidhiwa kwa Stamico miaka 10 iliyopita ukiwa na vifaa vyote.
Alisema awali mgodi huo ulikuwa ukilindwa na kampuni binafsi lakini baada ya kukabidhiwa serikalini ukaanza kulindwa na polisi na uligeuzwa ‘shamba la bibi’ kwa maelezo kuwa watu walianza kuondoa nyumba zilizoachwa na wawekezaji.
“Stamico imeshindwa lakini bado tumeendelea kuipa miradi ya kujaribu, hapa tumeona imekuwa ikiomba fedha kwa ajili ya miradi lakini imeendelea kuzalisha hasara na ina deni la Sh60 bilioni,” alisema Gulamali.
Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Naftaha Nachuma alionyesha kushangazwa na uwepo wa shirika hilo licha cha wabunge na kamati za Bunge kuzungumzia udhaifu wake. “Stamico imeshindwa kusimamia rasilimali za madini lakini leo tunasikitika Serikali kuendelea kulilea shirika hili wakati linatuingizia hasara Taifa,” alisema.
“Limeshindwa kusimamia madini yetu ya vito na mengine. Naomba nipate taarifa pamoja na kuliingizia hasara Taifa kwa nini bado Serikali inalibeba.”
Mbunge wa Newala Vijijini (CCM), Ajali Rashid Akibar aliungana na wenzake lakini yeye akienda mbali zaidi na kumtaka waziri wa wizara hiyo, Angellah Kairuki kwenda Afrika Kusini kuleta sangoma (waganga wa kienyeji) ili wasaidie upatikanaji wa madini, kwa maelezo kuwa baadhi ya madini hupatikana kwa imani za mashetani.
Huku akieleza kuwa wizara hiyo ina mawaziri watatu kutokana na Rais John Magufuli kuonyesha wasiwasi wa utendaji wake, aliwataka kufanya uamuzi mgumu kwa kuivunja Stamico kwa madai kuwa imeingia mkataba tata na kampuni ya TanzanineOne.
“Stamico ni mzigo kwenu. Wamekuwa ni tatizo walikuwa wanamiliki mradi wa makaa ya mawe wa Kiwara, wamechimba wamepata tani 8,000 wameuza wamepata Sh500 milioni,” alisema. “Hebu angalia ukubwa wa Stamico, tani 2,200 wameweka stoo. Na inasemekana tani hizo zilizoko stoo si chochote bali ni uchafu. Stamico ni shirika linaloingiza hasara. Ningekuwa mimi ni ninyi leoleo jioni ninge-declare (ningetamka) kulifuta. Nyinyi ni mawaziri vijana, mkiendelea kuwa nayo mtaondoka nayo.”
Kamati ya Bunge yalikomalia
Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini nayo imeishauri Serikali kufanya tathmini upya ya uwekezaji katika migodi yote iliyoridhiwa na Stamico ili kuona kama kuna faida na sababu za kuendelea na uwekezaji huo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dastan Kitandula alisema ni vyema maeneo hayo wakawapatia wachimbaji wadogo na wa kati ili waweze kuyaendeleza kuepusha migogoro isiyo ya lazima na wananchi wetu.
“Kama ilivyo migodi mingine inayomilikiwa na Stamico kurithi madeni makubwa kutoka kwa wawekezaji waliofunga shughuli zao hapa nchini, mgodi wa Buhemba unakabiliwa na deni la Sh89 milioni,” alisema Kitandula.
Alifafanua kuwa deni hilo linatokana na mapunjo ya mafao ya wafanyakazi wa zamani walioachishwa kazi mwaka 2007 wakati mgodi huo unamilikiwa na kampuni ya Meremeta.
Kitandula alisema kamati inashindwa kuelewa kwa nini wawekezaji wanapofunga shughuli zao katika migodi mingi mbalimbali wamekuwa wakiacha madeni makubwa ambayo hubebwa na Stamico wanapokabidhiwa na Serikali.
Alisema sintofahamu nyingine ya madeni hayo imeendelea kuwa mzigo kwa wizara na Serikali kwa ujumla kwa kuwa Stamico hutakiwa kuyalipa madeni hayo pale wanapokabidhiwa migodi pamoja na kuwepo na takwa la kisheria.
Alisema takwa la kisheria linawataka wawekezaji wote wanapofunga shughuli zao wanaacha mazingira katika hali nzuri na madeni yote yamelipwa hususan kodi na tozo mbalimbali za Serikali. Kamati hiyo pia iliitaka ofisi ya Waziri Mkuu kuingilia kati mgogoro wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na kampuni ya madini ya Cata kwa kuzikutanisha Wizara ya Madini na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kupata ufumbuzi wa haraka.
Fedha kiduchu zilipokewa
Awali akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo, Kairuki alisema katika mwaka wa fedha 2017/18 walitengewa Sh52.44 bilioni, kati ya fedha hizo za maendeleo zilikuwa ni Sh21.8 bilioni.
Hata hivyo alisema hadi kufikia Machi 30 wizara hiyo ilikuwa imepokea Sh834.97 milioni sawa na asilimia 3.83 ya bajeti yote ya maendeleo.

Comments