Ukuta mgodi wa Tanzanite waongeza mapato ya mrabaha hadi 714 milioni

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akiwasilisha

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma jana. 
Dodoma. Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amesema ujenzi wa ukuta unaozunguka mgodi wa madini ya Tanzanite, umewezesha Serikali kukusanya mrabaha mara tatu zaidi ya ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita.
Waziri Kairuki alisema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2018/19, iliyoanika mikakati ya wizara yake ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na shughuli za madini.
Wizara hiyo ambayo sasa imetenganishwa na Nishati, imeliomba Bunge kuidhinisha Sh58.9 bilioni kwa ajili ya matumizi yake ya mwaka 2018/19, hilo likiwa ni ongezeko la Sh6.5 bilioni ikilinganishwa na bajeti iliyopita.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, kati ya fedha hizo, Sh19.6 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Sh39.2 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Kairuki alisema bungeni mjini Dodoma jana kuwa ukuta huo ambao ujenzi wake ulianza Novemba 1, 2017 na kukamilika Februari 15 umeongeza mapato, akibainisha kuwa katika kipindi kifupi cha Januari hadi Machi, 2018 wizara ilikusanya jumla ya Sh714.6 milioni.
Alisema kati ya fedha hizo, Sh614.7 milioni zinatokana na makusanyo kutoka kwa wachimbaji wadogo.
Mbunge huyo wa viti maalumu (CCM) alisema kiasi hicho kinazidi jumla ya makusanyo ya mrabaha wa miaka mitatu iliyopita.
Alisema katika mwaka 2015, Serikali likusanya mrabaha wa Sh166.9 milioni, 2016 Sh71.9 milioni na mwaka 2017 ilipata Sh147.1 milioni kutoka kwa wachimbaji wadogo.
Kairuki alisema wizara itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na shughuli za madini na lengo la mwaka 2018/19 ni kukusanya Sh310.5 bilioni.
Makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 59.57 ikilinganishwa na Sh194.7 bilioni zilizopangwa kukusanywa 2017/18.
“Wizara inatarajia kuimarisha ukaguzi wa migodi mikubwa, ya kati na ya uchimbaji mdogo ili kupata taarifa sahihi za uwekezaji, uzalishaji, mauzo na kodi mbalimbali na kudhibiti utoroshaji wa madini katika maeneo ya uzalishaji,” alisema.
Kairuki alisema wizara itaendelea kuhamasisha uwekezaji na shughuli za uongezaji thamani madini pamoja na kuendelea kutoa leseni za uchenjuaji na uyeyushaji wa madini ya metali.
“Wizara itakamilisha kazi ya kuwapata wawekezaji katika vinu vya uchenjuaji na usafishaji wa madini. Wizara itaandaa muswada wa sheria ya uongezaji thamani wa madini ili kusimamia vyema uongezaji thamani madini nchini,” alisema
Kairuki alisema viwanda vya uyeyushaji, usafirishaji wa madini na shughuli nyingine za uongezaji thamani zinatarajiwa kuongeza mapato, ajira na kukuza matumizi ya teknolojia nchini.
Alisema mwaka 2018/19, wizara yake itaandaa muswada wa kurekebisha Sheria ya Baruti ya mwaka 1963 na kanuni zake za mwaka 1964; Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2015 na Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017.
Akigusia wachimbaji wadogo, Kairuki alisema wizara itaendelea kutekeleza mpango wa kuwaendeleza kwa kutenga maeneo yanayofaa na wanatarajia kutenga maeneo manne kwa shughuli hiyo.
Alisema Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (Teiti) itatoa kwa umma ripoti ya malipo ya kodi iliyofanywa na kampuni za madini, mafuta na gesi kwa kipindi cha mwaka 2016/17.
Alisema Teiti itaanzisha rejista ya taarifa na majina ya watu wanaomiliki hisa katika kampuni za madini, mafuta na gesi asilia.

Comments