Ugumu wa kazi wa Dk Bashiru ni zaidi ya ukatibu mkuu CCM
Katibu Mkuu wa CCM Dk Bashiru Ally, akizungumza na wajumbe wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa NEC wakati akiwasilisha Ripoti ya uhakiki wa mali za Chama cha Mapinduzi CCM kwa wajumbe hao Ikulu jijini Dar es Salaam juzi
Kuna kuwa katibu mkuu CCM na katibu mkuu baada ya Abdulrahman Kinana. Ni kama ambavyo kulikuwa na urais wa Tanzania na urais baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Ukiwaza hivyo, utajua ni kiasi gani Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi alipata ugumu kumrithi Nyerere.
Juni 7, mwaka jana, mwandishi wa Alberta, Canada ambaye pia ni mchambuzi wa siasa na uchumi, Jason Markusoff, aliandika makala kwenye jarida la Maclean’s, yenye kichwa: “Missing Barack Obama, and his long, hard march toward change.”
Tafsiri yangu: “Kumkosa Barack Obama na falsafa zake, matembezi magumu kuelekea mabadiliko.” Andiko hili lilichapishwa siku 13 kabla ya Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump hajatimiza miezi mitano ofisini. Ukimwelewa Markusoff utapata picha kwamba kuna urais wa Marekani na urais baada ya Obama.
Markusoff aliandika kwamba alama ya urais wa Obama ni kuwa wazo la mabadiliko ya kisiasa ni mradi mgumu kila siku unaohitaji uvumilivu na muda. Alimfananisha na Trump kuwa yeye kila kitu anachukulia kwa wepesi. Yaani kwake kila kitu ni rahisi kuamua na kutenda.
Ni kama ambavyo ukisoma maandishi ya mwandishi wa habari wa Marekani, Kenneth T. Walsh pamoja na yale ya mwanahistoria, Doris Kearns Goodwin, kuhusu Rais wa 32 wa Marekani, Franklin Roosevelt, yatakuelekeza kutambua kuwa kuna urais wa Marekani na urais baada ya Roosevelt (FDR).
Kiongozi ambaye aliikuta nchi ikiangamia kwa mdororo mkubwa wa kiuchumi na anguko la viwanda. Akaweza kuiimarisha na kuifanya nchi hiyo kuwa taifa lenye nguvu za kiuchumi duniani. Unaweza kujionea mwenyewe kwamba kumrithi FDR kwa usahihi ilihitaji mtu mwenye sifa maalum.
Kwa ufafanuzi huo, bila shaka sasa naeleweka nikisema kuwa kumrithi Kinana kama Katibu Mkuu CCM na kuvaa viatu vyake kwa usahihi si kazi nyepesi. Inahitaji mtu mwenye maarifa, utashi na kipawa. Dk Bashiru anaweza, lakini vema akumbushwe hata kama anajua, kwamba ukatibu mkuu CCM baada ya Kinana ni mgumu mno.
Ugumu uliopo
Dk Bashiru amepokea kijiti cha ukatibu mkuu CCM kutoka kwa mtu mwenye kuaminika mtu. Kinana ana haiba kubwa kisiasa. Ni kiongozi wa muda mrefu, na kwa hakika aliingia ofisini kipindi chama kikiwa na misukosuko mingi, zaidi alifanikiwa kukivusha salama kwenye uchaguzi.
Kinana aliingia kuwa Katibu Mkuu CCM kwa maombi maalum ya Mwenyekiti aliyepita, Jakaya Kikwete aliyeomba nguvu ya ushawishi kutoka kwa wazee. Wenyeviti waliotangulia kabla ya Kikwete, Benjamin Mkapa na Mwinyi, wanatajwa kubeba nguvu ya ushawishi, iliyomfanya Kinana akubali kukitumikia chama.
Kutokana na kuaminika huko, maana yake Kikwete na wazee wa CCM walibeba matarajio makubwa kwamba Kinana alikuwa na hadhi, uwezo na vigezo vingi vya kuiwezesha CCM kuvuka salama nyakati ngumu za kisiasa ambazo chama hicho kilikuwa kinapitia ndani na nje.
Ndani ya CCM kulikuwa na minyukano miwili. Mmojapo ni ule ulioanzia mwaka 2008 baada ya Ripoti ya Richmond kusomwa bungeni na kumng’oa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa pamoja na mawaziri wawili, Nazir Karamagi (Nishati na Madini) na Dk Ibrahim Msabaha (Afrika Mashariki).
Waliokumbwa au kutajwa kwenye Ripoti ya Richmond pamoja kashfa nyingine zilizoainishwa kama ufisadi, waliunda upande wao ambao unaweza kuuita wa waathirika wa tuhuma za ufisadi, kundi la pili walijipambanua kama makamanda au wapiga vita ufisadi.
Mnyukano wa makundi hayo mawili, ulisababisha mtikisiko mkubwa CCM. Zaidi, mvurugano huo ulikuwa sababu ya chama hicho kutetereka na kupoteza imani kwa wananchi. Wanachama na viongozi wa CCM wenyewe waligawanyika na kunyukana waziwazi na kuzidi kukipa sifa mbaya chama chao.
Mnyukano wa pili ni mchuano wa urais kuelekea mwaka 2015. Zipo nadharia zenye kuutaja hata mnyukano wa makundi ya waathirika tajwa wa ufisadi na makamanda wa ufisadi kuwa chanzo chake ni mbinu za kuzidiana kasi kuelekea kumrithi Kikwete ambaye ni Rais wa awamu ya nne wa Tanzania.
Kwamba katika kuchafuana na kuharibiana sifa za kukielekea kiti cha urais baada ya Kikwete, upande mmoja ulibeba bango kuhusu ufisadi na kushambulia wenzao. Kundi lingine lilidaiwa kucheza rafu nyingi za kimkakati ili kuhakikisha linachukua hatamu ya uongozi wa nchi kwa namna yoyote.
Likaibuliwa lingine baada ya Uchaguzi Mkuu 2010 la kujivua gamba. Kikwete alitumia nadharia ya nyoka, akizeeka hujivua gamba na kurejea kuwa kijana, kwamba CCM nayo ilitaka kujivua gamba ili kuwaondosha watu wote wenye kashfa za ufisadi, kusudi chama kionekane kipya na kisafi mbele ya Watanzania.
Watu ambao walikuwa wakitajwa kuwa ni magamba wenye kustahili kuvuliwa ili CCM iwe mpya ni watu wazito wenye ushawishi mkubwa. Vinara wao walikuwa Lowassa na swahiba wake, Rostam Aziz. Hivyo, kadiri walivyosemwa na kutishiwa kufukuzwa, chama kiligawanyika na kukuza mpasuko.
Alipoondoka Yusuf Makamba kama katibu mkuu Aprili 2011 na nafasi yake kuchukuliwa na Wilson Mukama, ilidhaniwa ndiyo ungekuwa mwanzo wa CCM mpya, kwani sekretarieti yote ilibadilika. Kinyume chake CCM kilipitia kipindi kigumu cha mwaka mmoja na miezi saba, na kufanya chama kizidi kupoteza nuru.
Changamoto kubwa nyingine kwa CCM ni kukua kwa upinzani, hasa Chadema. Kadiri CCM walivyokuwa wananyukana wao kwa wao, ndivyo upinzani ulivyostawi na kuvuna imani ya mamilioni ya Watanzania. Kipengele hiki kinachukuana na ukweli kuwa wapinzani walikuwa na timu nzuri.
Mathalan, Chadema safu yao ya uongozi iliundwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Willibroa Slaa, Naibu Katibu Mkuu Bara, Zitto Kabwe, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, John Mnyika, mwanasheria na mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu na wengine.
Chadema ilipata mavuno ya watu wazito kwenye siasa za Tanzania; Profesa Mwesiga Baregu, Mabere Marando, Profesa Abdallah Safari, Arcado Ntagazwa na wengine ambao walichangia uzoefu wa kisiasa na kusababisha chama hicho kionekane ni chenye kukomaa haraka.
Hivyo, Kinana alikuwa na jukumu la kurejesha chama kwenye ukubwa wake. Kiti cha Katibu Mkuu alichokalia, cha upande wa pili kilikaliwa na Dk Slaa. Hapo tu ilikuwa kuonesha ni kiasi gani mapambano hayakuwa mepesi. Mapambano dhidi ya mwenye nguvu yanataka uwezo, kujiamini na mbinu za ziada.
Katikati ya changamoto hizo, Kinana alichomoza, akafanikiwa kukipa uhai chama. Akawafanya wananchi waone CCM ni chama mali yao, aliunganisha makundi si kwa kuwasuluhisha, bali kwa vitendo vyake vilivyotoa tafsiri kuwa kila mwanachama aijenge CCM na si kubomoa.
Turufu kubwa ambayo Kinana hawezi kunyimwa ni namna alivyowezesha CCM kushinda urais mwaka 2015, licha ya mgawanyiko mkubwa uliotokea, hasa kitendo cha Lowassa kuhama na kwenda kugombea urais kwa tiketi ya Chadema. Haikuwa kazi rahisi hata kidogo.
Wajibu wa Bashiru
Sifa za utukufu anazokuwa nazo mtangulizi ni mzigo kwa mrithi wake. Hivyo, Dk Bashiru anapaswa kuangalia uhusika wa Kinana kama wajibu nambari moja. Akifanya chini ya kiwango, kila mmoja atamsema kuwa amepwaya. Na anatakiwa kutambua kwamba hawezi kukwepa kupimwa na Kinana.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, mpaka leo anaendelea kupimwa na Slaa. Ni kwa sababu Slaa aling’ara mno kwenye ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema. Kumekuwa na minong’ono mingi kutoka kwa wana Chadema kuwa Dk Mashinji hatoshi ukatibu mkuu, ni kwa sababu anapimwa na Slaa.
Tukishakubaliana kuwa Dk Bashiru hawezi kukwepa kupimwa na Kinana, ushauri kwake ni kutazama yapi ambayo yaliwafanya viongozi na wanachama CCM kumuona Kinana ni wa kipekee kiasi cha kutotaka aondoke licha ya yeye mwenyewe kuomba kwa msisitizo kuachia ngazi miaka miwili mfululizo.
Umahiri wa Kinana haupo kwa namna alivyoijenga CCM kimuundo, bali alijiuza kikamilifu kwa wanachama na wananchi kwa jumla. Alikifanya chama kibebe sura ya utetezi wa maisha ya watu. Dk Bashiru ili afikie daraja hilo inabidi afanye kazi kweli. Atoke na kukutana na wananchi.
Kipindi hiki Rais John Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa chama chake amepiga marufuku shughuli za kisiasa, hasa mikutano ya hadhara, itamuwia vigumu Dk Bashiru kuvivaa viatu vya Kinana na kumtosha. Labda amshauri kwanza mwenyekiti wake aruhusu shughuli za wazi za kisiasa ili naye achape kazi.
Wajibu mwingine wa Dk Bashiru kama Katibu Mkuu CCM ni kutoa matokeo bora Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020. Hivi sasa shughuli za kisiasa hazifanyiki, kwa hiyo inakuwa vigumu kupata tathmini iliyo karibu na ukweli kuhusu kubalika au kutokukubalika kwa chama.
Nyakati kama hizi, watu wengi wanaficha hisia zao nyoyoni. Watazionesha wakati wa kampeni za uchaguzi. Hivyo, ni vigumu sana kupata picha juu ya kukubalika au kutokukubalika kwa chama. Huu ni mtihani mkubwa ambao Dk Bashiru lazima aufanye na afaulu.
Jaribio la kwanza ni uchaguzi mdogo jimbo la Buyungu, Kigoma, baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Kasuku Bilago. Hilo lilikuwa jimbo la Chadema, hivyo akikiwezesha chama chake kushinda, atakuwa ameingia kwa mguu mzuri wa kurejesha jimbo ambalo CCM ililipoteza mwaka 2015.
Mzigo mkubwa zaidi alionao Dk Bashiru ni wasifu wake. Ni msomi wa sayansi ya siasa na uongozi wa umma na amefundisha masomo hayo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Zaidi amekuwa mchambuzi mahiri wa masuala ya siasa nchini na kimataifa. Hivyo alijipambanua vizuri na watu wanatarajia makubwa kutoka kwake.
Hata hivyo, uwezo wa kuchambua si wa kutenda. Beki wa zamani wa Manchester United na Timu ya Taifa ya England, Gary Naville ni mchambuzi hodari mno wa soka. Desemba 2015 alipewa kazi ya ukocha wa Klabu ya Valencia, Hispania. Hakudumu hata miezi minne, alitimuliwa. Ni kwa sababu kuchambua si kutenda. Dk Bashiru afanye kazi sana.

Comments
Post a Comment