Ripoti ya Bunge yawaweka mtegoni mawaziri



Dodoma. Kama ripoti ya Kamati Maalumu ya Bunge kuhusu madini ya Tanzanite na almasi iliwaondoa mawaziri, kwa nini isiwe ripoti ya kamati ya gesi asilia na uvuvi wa bahari kuu?
Ndivyo inavyoonekana baada ya Kamati ya Kuchunguza Gesi Asilia na Uvuvi katika Bahari Kuu iliyoundwa na Spika Job Ndugai kukabidhi ripoti zake jana, ikionyesha hasara ya matrilioni ya fedha na kuhusisha mawaziri na watendaji.
Mawaziri waliong’oka baada ya ripoti ya uchunguzi wa biashara ya almasi na Tanzanite ni George Simbachawene na Edwin Ngonyani kutokana na nafasi zao walizoshikilia katika Serikali ya Awamu ya Nne.
Wengine waliotajwa katika ripoti hizo za mwaka jana ni waliowahi kuwa mawaziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na William Ngeleja.
Na sasa, kuna kila dalili mawaziri wengine wakawajibika au kujiwajisha baada ya ripoti ya kamati maalumu za Bunge kuwahusisha kufanya uamuzi unaokiuka sheria au kusababisha upotevu wa fedha hizo.
Ripoti hizo mpya zilikabidhiwa kwa Spika Ndugai ambaye alizikabidhi moja kwa moja kwa kaimu kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Profesa Makame Mbarawa.
“Tumeyasikia mengi. Watanzania wamesikia mengi kuhusu ripoti hizi. Tutasoma ripoti hizi neno kwa neno, mstari kwa mstari na kipengele kwa kipengele,” alisema Profesa Mbarawa baada ya kupokea ripoti hizo.
“Kuna mengi yamesemwa, lakini niwahakikishe Bunge na Watanzania kwamba, mapendekezo yote tutayatekeleza kwa haraka.”
Waliotajwa katika ripoti ya kamati ya gesi asilia, iliyoongozwa na Dunstan Kitandula ni mawaziri wa zamani; Edgar Maokola Majogo, Abdallah Kigoda (marehemu) na Daniel Yona ambao walikuwa katika Serikali ya Awamu ya Tatu.
Katika awamu ya nne waliotajwa ni Naziri Karamagi na William Ngeleja aliyetajwa katika mikataba mitatu sawa na Daniel Yona pamoja na aliyekuwa mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC), Yona Kilagane aliyetajwa katika kila mkataba.
Dk Charles Tizeba, ambaye ni waziri wa Kilimo pia ametajwa kutokana na nafasi yake ya awali wakati wizara hiyo ikihusisha pia Mifugo na Uvuvi, pamoja na Hamad Rashid ambaye ni waziri wa Afya Zanzibar. Rashid ametajwa kutokana na nafasi yake ya awali kama waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi.
Hao wanahusishwa na sakata lililosababisha Serikali kupata hasara ya Sh5.45 bilioni kutokana na uamuzi wao wa kusitisha leseni za uvuvi kinyume cha sheria.
Kamati ya Gesi Asilia
Akiwasilisha ripoti hiyo jana kwenye viwanja vya Bunge, Kitandula alisema mikataba mingi iliyopitiwa na kamati yake ilikuwa na utata na akapendekeza Serikali kuangalia upya kwa kuwa baadhi inapaswa kusitishwa mara baada ya kumalizika kwa muda wake.
“Kuna mikataba kumi na moja ya utafutaji na uendeshaji wa gesi. Awali mikataba ilikuwa 26 lakini wengine walirudisha baada ya kuona hakuna masilahi na kwa sasa mikataba mitatu iko kwenye uzalishaji wakati mikataba minane iko hatua za utafiti na ugunduzi,” alisem.
Kitandula ambaye ni mbunge wa Mkinga (CCM), alitaja mkataba wa Songosongo kuwa miongoni mwa mikataba yenye utata zaidi ambao unapaswa kuangaliwa akisema una shida kubwa.
Mkataba huo pia ulilalamikiwa na mbunge wa viti maalumu, Jesca Kishoa (Chadema) wakati wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati. Kishoa alisema Serikali inateketeza mabilioni kwa kulipa watu bila msingi wowote.
“Katika kampuni ya Pan Africa Energy Tanzania tumekuta mtu analipwa mshahara wa Sh96 milioni wakati Watanzania wenye nafasi kama yake wanalipwa mshahara huo watu wanne, sisi tumeona ni ujanja wa kusafirisha pesa nje,” alisema Kitandula.
“Katika eneo jingine, watumishi watatu walitumia Sh106 milioni kulipana bonansi kwa miezi mitatu wakati Serikali imepata hasara kubwa katika eneo hilo la kiasi cha Sh291.9 bilioni.”
Kitandula alisema katika kipindi kifupi eneo hilo lilipoteza mapato ambayo yanalingana na bajeti za wizara tano zilizowasilishwa bungeni kwa mwaka 2018/19, lakini alizitaja nne ambazo ni Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira); Habari, Utamaduni, Sana na Michezo; Madini na ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji huku bomba la Songas likitafuna Sh19 bilioni zinazoelezwa kuingizwa katika ujenzi, lakini hakuna ushahidi.
Alisema baadhi ya viongozi wa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini hawakuwa na nia njema kwa Serikali yao, lakini cha ajabu bado hawajachukuliwa hatua. Aliomba Serikali iwachunguze wahusika wote ili kujiridhisha kama walikuwa na nia njema au walifanya kwa makusudi.
Kamati ya Uvuvi Bahari Kuu
Kuhusu uvuvi wa bahari kuu, mwenyekiti aliyeongoza kamati hiyo, Anastazia Wambura alisema Tanzania ilipoteza Sh5.98 trilioni katika kipindi cha miaka tisa (2009-2017) kutokana na ubovu wa sheria za uvuvi na kusitishwa kwa utoaji wa leseni za uvuvi kinyume cha sheria huku Mamlaka ya Mapato (TRA) ikishindwa kutafsiri sheria ya kodi
Kati ya hasara hizo, Sh5.42 bilioni zilisababishwa na uamuzi wa waliokuwa mawaziri wa sekta hiyo, Dk Tizeba na Hamad Rashid kusitisha leseni za uvuvi kinyume na sheria.
Wengine ni Boniface Damian Chande na Ahmed Husseinali Shaaban, ambao ripoti imesema waliisababishia Serikali hasara kwa kugushi leseni za uvuvi. Ripoti inasema kwa miaka sita wawili hao wametajwa kuhusika kuisababishia Serikali hasara ya Sh50.23 bilioni, lakini hawajakamatwa.
Wambura, ambaye ni mbunge wa viti maalumu (CCM), alisema kamati inapendekeza baadhi ya watendaji ndani ya Wizara ya Uvuvi na Mifugo wachunguzwe kwa kuwa kuna viashiria vya uzembe uliotokana na utendaji wao na pia imeshauri kitengo cha majini cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kusaidia kulinda bahari kuu.
“Tulishangazwa na hotuba ya waziri wa Mifugo na Uvuvi (Luhanga Mpina) kwamba kuna meli 24 zilikuwa zimeingia bahari kuu na kutoa bai kachi lakini akasema meli tano ndizo zilitoa lakini eti meli 19 zilitoroka,” alisema.
“Hapa kuna shaka. Tunaomba uchunguzi ufanyike maana gharama za leseni ni hadi Dola 80 milioni (za Kimarekani). Haiwezekani kupata meli ambazo zinakuja kuuza bai kachi kwa Sh2 au 3 milioni kama si uvuvi haramu ni nini?”
Mbarawa: Tutatekeleza yote
Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hizo, Profesa Mbarawa alisema watatekeleza mapendekezo yote yaliyo kwenye ripoti hiyo.
Profesa Mbarawa alisema amesikiliza ripoti hizo na kubaini kuna shida katika mikataba hasa gesi na kwamba asilimia kubwa ni kasoro.
“Utasikia kuna kasoro, kasoro katika mikataba na Serikali ya Awamu ya Tano tumelisikia na tumejipanga na tutafanyia kazi,” alisema.
“Kama ambavyo ripoti zimeeleza, wale ambao walihusika tutafanya uchunguzi na sheria itachukua mkono wake.”
Alisema kuna shida ya sera, kanuni na sheria katika sekta ya uvuvi na kuahidi kuwa Serikali itazifanyia kazi ili uvuvi uwe na masilahi kwa Taifa.
Kuhusu watu wawili walioisababishia harasa Serikali, Mbarawa alisema hilo ni suala la vyombo vya dola.
“Kuna watuhumiwa wawili wametajwa. Vyombo vya dola vitachukua hatua kwa wale walioghushi leseni za uvuvi,” alisema.
Spika Ndugai
Awali, kabla Spika Ndugai hajakabidhi ripoti hizo, alisema aliamua kuunda kamati hizo kama alivyofanya kwa kamati za Tanzanite na alamas ili kutekeleza nia ya Bunge ya kuishauri na kuisimamia Serikali.
Alisema hatua hiyo ni kuunga mkono jitihada zilizoanzishwa na Rais John Magufuli za kusimamia rasilimali za Taifa na kuhakikisha zinawanufaisha Watanzania na akawaomba wananchi wamuunge mkono.
Ndugai alisema matokeo ya kamati ya Tanzanite na almasi yameanza kuonekana kwa kuwa mauzo ya Tanzanite yamepanda maradufu. Alisema almasi katika mgodi wa Mwadui mkoani Shinyanga bado ipo kwa kwango cha asilimia 70 ardhini. “Kama tungekuwa sawa, tusingekuwa hapa tulipo. Nimpongeze Rais wetu, jambo hili si jepesi. Hapa tunashughulika na majitu yenye fedha nyingi, yamebaki kutununua tu,” alisema Spika Ndugai.
“Tumempata kiongozi. Katika Ikulu yake hakuna hata mmoja anayekanyanga, lazima tumuunge mkono na wale wanaotupinga wakae sawa ila mwendo ni huo huo.”
Alisema tatizo kubwa liko katika mikataba. “Mikataba imetuumiza sana, sana. Hii kampuni ya Songas na mambo yake ni kampuni nyonyaji. Kupitia mikataba ya hovyo wameitwisha Tanesco mizigo ya ajabu kwa kushirikiana na kampuni ya Pan African Enegy,” alisema.
“Kampuni hizi zimeiumiza sana TPDC kwa kuitwisha masharti ya ajabu ikiwamo kuibebesha gharama za uendeshaji.”
Ndugai alisema katika biashara ya gesi Taifa litafaidika kupitia TPDC.
“Unafika mahali visima vyote vya Songosongo unampa bure tu Songas, lazima uwe umerogwa. Yako mambo huwezi kufanya hivi hivi.”

Comments