Maonyesho Sabasaba yanukia, kampuni 2400 kushiriki
Dar es Salaam.Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tanrade) imetangaza kuanza kwa siku 16 za maonyesho ya biashara huku kampuni 2456 zikithibitisha kushiriki.
Akizungumza leo Juni 1, Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, Edwin Rutageruka amesema asilimia 89.4 ya eneo la maonesho limeshakodishwa.
Amesema maonesho hayo yataanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu na kampuni za nje zilizothibitisha kushiriki hadi sasa zikiwa ni 450.
Amesema taasisi za serikali 120 zitashiriki katika maonesho.
Amesema maandalizi ya kukarabati majengo yatakamilika kati juni 21 na 22.
"Tunawaomba waliochukua mabanda kwa ajili ya maonesho kufanya maandalizi mapema" amesema.
"Haipendezi muda wa maonesho umeanza watu wanapanga bidhaa," amesema.
Amesema ratiba za ufunguzi na ufungaji zitatangazwa baadaye baada ya kukamilika kwa mawasiliano na mamlaka za juu.
Kauli mbiu ya maonesho ya 42 ni ukuzaji biashara kwa maendeleo ya viwanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa huduma ya taasisi wa Tantrade, Martha Paul amewataka wafanyabiashara wanaotaka maeneo ya kukodi kuwahi vinginevyo watayakosa.
"Kama ilivyoelezwa asilimia 89.4 ya majengo ya Tanrade yameshakodishwa mkiendelea kuchelewa mtayakosa" amesema

Comments
Post a Comment