Iringa watakiwa kuwataja wauza dawa za kulevya



Iringa. Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa ya Kulevya, Rogers Sianga amewataka wakazi wa Iringa kutoa taarifa za wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya ili wachukuliwe hatua.
Sianga amesema hayo wakati wa uzinduzi wa matembezi ya wiki ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya iliyofanyika leo Juni 22 katika eneo la Ngome mkoani hapa.
“Tunaomba mtusaidie kuwapata wauzaji ambao inadaiwa wameshindikana hao ndio tunaowatafuta ili tuwachukulie hatua kali kwa sababu ndio wanaoaribu vijana wa taifa hili,” amesema.
Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza amesema mkoa huo  umepata fursa ya kuelimishwa kwa upana  zaidi juu ya madhara  ya matumizi ya dawa hizo.
“Wananchi tutambue tumepewa jukumu kubwa hivyo tuunganishe nguvu zetu kama ilivyo kawaida yetu ili kuithibitishia Tanzania kuwa tukipewa kazi tunaweza kuisimamia,” amesema.
Masenza amewaomba vijana ambao kwa njia moja au nyingine wanajihusisha au wanashawishiwa kuingia kwenye dawa za kulevya wajue taifa hili linawathamini.
 “Hatuwezi kuingia kwenye ujenzi wa viwanda kumuunga mkono Rais John Magufuli tukiwa na kundi kubwa la vijana wanaotumia madawa ya kulevya,”amesema Masenza.
Amesema madawa ya kulevya ni sumu inayowaua vijana polepole na inapunguza nguvu kazi ya taifa.



Comments

Popular Posts