Wingu zito saa 48 vikao vya CCM





Dar es Salaam. Wakati kesho CCM ikitarajia kuanza vikao vyake vya juu vya chama, huenda kukatokea maamuzi mazito saa 48 zijazo.
Vikao hivyo ni vya Kamati Kuu (CC) pamoja na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vitakavyofanyika kwa siku mbili; Jumatatu na Jumanne huku baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wakibashiri kuwapo kwa maamuzi mazito.
Hivi karibuni, mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli akipokea ripoti ya uchunguzi wa mali za chama hicho alitoa ahadi ya kuipeleka katika vikao hivyo ili kuijadili na kutoa maamuzi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema jana kuwa, “nadhani watajadili ripoti kuhusu uhakiki wa mali za CCM iliyowasilishwa hivi karibuni na kamati iliyoteuliwa na Rais John Magufuli. Juzi tu tulishuhudia wenyeviti wa jumuiya tatu za CCM wakitoka Ikulu baada ya kufanya mazungumzo na rais.”
“Tutarajie vikao hivyo vitachukua hatua kali kwa wale watakaobainika kujinufaisha na mali za CCM ili iwe fundisho kwa viongozi wa chama hicho.”
Kwa upande wake, balozi mstaafu Dk Ahmed Kiwanuka alisema kama uamuzi upo huenda ukafanywa kwa kuwa vikao hivyo vipo kikatiba.
“Wanaweza wakafanya uamuzi kwa kuzingatia katiba ya chama na itategemea zaidi na ajenda zitakazojadiliwa. Kwa vyovyote wajumbe wa vikao hivi hawataogopa kutoa uamuzi,” alisema Dk Kiwanuka ambaye aliwahi kuwa mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia vikao hivyo, makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alisema, “watajadili mambo kadhaa likiwemo pendekezo la Rais kuwaongeza wajumbe wawili, waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda na Makongoro Nyerere.
“Kwa hiyo wajumbe wana hiari ya kuwakataa au kuwakubali. Kwa vyovyote watakubaliwa kwa sababu haijawahi kutokea mapendekezo ya mwenyekiti yakakataliwa.”
Ukimya juu ya Kinana
Wakati wachambuzi wakieleza hayo, kumekuwapo na maswali mengi juu ya ukimya wa katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Kwa takribani siku kadhaa, Rais Magufuli amekuwa akikutaka na viongozi mbalimbali wa chama hicho tawala, lakini Kinana hajaonekana kwenye taarifa zilizotumwa na Ikulu kwa vyombo vya habari kama mmoja ya waliokutana na Rais.
Juzi, Magufuli alikutana na Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa pamoja na makamu mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Philip Mangula, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Vilevile alikutana na wenyeviti watatu wa jumuiya za chama hicho akiwamo Gaudentia Kabaka (Wanawake), Edmund Mndolwa (Wazazi) na Kheri James (Vijana).
Jana, Dk Magufuli alikutana na Mangula pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ambaye pia ni makamu wake upande wa Zanzibar, huku taarifa iliyotolewa na Ikulu ikisema wamezungumzia mambo mbalimbali kuhusu chama na Serikali.
Licha ya kutotajwa katika taarifa hizo za juzi na jana, Kinana alionekana Mei 11, pale Rais Magufuli na Mangula walipokutana kwa mazungumzo katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM zilizopo Lumumba.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba hivi karibuni alikuwa Afrika Kusini ambako alikitembelea chama cha ANC akiwa na viongozi wa jumuiya za CCM.
Wakati Kinana akiwa haonekani mara kwa mara, hivi karibuni katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole alifanya ziara ya kichama katika mikoa mbalimbali nchini huku akipokea wanachama wapya.

Comments