Ukipoteza hati ya kusafiria, utaipata kwa Sh500,000



Dar es Salam. Mtanzania atakayepoteza hati ya kielekroniki ya kusafiria inayopatikana kwa Sh150,000 atalazimika kulipa Sh500,000 kupata mpya.
Pia, iwapo ataipoteza tena atalipa Sh750,000 ili aweze kupata nyingine.
Tayari hati za kusafiria za kielektroniki 15,101 zimeshatolewa kwa Watanzania tangu kuanza kwa utoaji huo Januari mwaka huu.
Kamishna wa Uhamiaji, Uraia na Pasipoti, Gerald Kihinga alisema hayo jana katika uzinduzi wa utoaji wa hati hizo Dar es Salaam na kuongeza kuwa gharama hiyo itasaidia watu kutunza hati zao.
Alisema zipo kesi nyingi za watu kupoteza hati zao za kusafiria na baadhi yake ni zile zinazotokea katika matukio yasiyohitaji uwapo wake.
“Utakuta mtu anakuja kuomba hati mpya, ukimuuliza mazingira (ilivyopotea) anasema alikuwa akielekea Kariakoo kutoka Buguruni, sasa huko Kariakoo hati hiyo unaenda nayo ya nini? Tuzitunze hati hizi kwa sababu ni nyaraka muhimu kwa nchi yetu,” alisema Kihinga.
Alifafanua kuwa hakuna haja ya kuzunguka na hati hiyo kila mahali isipokuwa yale maeneo muhimu yanayohitaji uwapo wake kuepuka gharama kubwa ya upatikanaji wake wakati inapopotea.
Pia, alieleza kuwa tangu kuanza kutolewa kwa hati hizo hakuna changamoto zilizojitokeza zaidi ya kuwapo baadhi ya watu wanaotumia mawakala kupata hati na hivyo kutozwa zaidi ya Sh300,000.
“Niwasihi tu wasitumie mawakala hawa, waende wao wenyewe kupata huduma hii, inatolewa kwa muda mfupi ikilinganishwa na hapo zamani hakuna usumbufu na kuwatumia mawakala,” alisema.
Kamanda wa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Chrispin Ngonyani alisema upo udhibiti wa kutosha kuhakikisha kila anayeomba hati hiyo anapewa kwa wakati bila bugudha wala usumbufu wowote.
Awali, akizindua hati hizo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema badala ya kulipa gharama kubwa kupata hati hiyo baada ya kuipoteza ni vizuri Watanzania kujenga tabia ya kuzitunza zidumu kwa muda mrefu.

Comments