Mawakili wachuana kila mmoja upande wake kesi mauaji ya Bilionea Msuya


Upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavulla, umeiomba mahakama kuwatia hatiani washtakiwa kwa vile ushahidi dhidi yao haukuacha mashaka.

Moshi. Mawakili wa utetezi katika kesi ya mauaji ya bilionea Erasto Msuya, wameiomba mahakama kuwaachia huru washtakiwa, wakidai ushahidi wa mashtaka umeacha mapengo mengi, kuhitilafiana na kukosa viwango vya kisheria kuwatia hatiani.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavulla, umeiomba mahakama kuwatia hatiani washtakiwa kwa vile ushahidi dhidi yao haukuacha mashaka.
Hayo yalijitokeza jana mbele ya Jaji Salma Maghimbi, wakati mawakili wa pande zote walipokuwa wakiwasilisha majumuisho ya mwisho ya kesi hiyo ambayo usikilizaji wake umechukua miaka mitatu.
Mawakili wa utetezi; Majura Magafu, Husdon Ndusyepo, Emmanuel Safari na John Lundu, walidai hakuna mshtakiwa aliyetoa maelezo kwa hiari yake bali wote waliteswa wakiwa mikononi mwa polisi.
Mbali na hoja hizo, mawakili hao walihoji kama maelezo ya kukiri kosa ya mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed ni ya kweli, iweje wanaotajwa kuwa vinara si miongoni mwa washtakiwa.

Katika maelezo hayo yaliyopokelewa kama kielelezo, Sharifu ananukuliwa akimtaja mfanyabiashara, Joseph Mwakipesile maarufu kama Chussa na mtu mwingine anayetajwa kwa jina moja tu la Kaburu.
Akiwasilisha majumuisho ya mwisho kwa niaba ya wenzake mbele ya Jaji Maghimbi, Magafu alidai mshtakiwa hakuwahi kukiri na maelezo hayana ukweli.
“Ukisoma hii statement (maelezo) ya Sharifu kuna watu wanatajwa kuwa walikuwa ring leader (vinara). Kuna Joseph Mwakipesile au kwa jina maarufu Chussa na mtu anayeitwa Kaburu.
“Kama ni kweli mshtakiwa aliwataja hao watu, je Kaburu na Chussa ni miongoni mwa washtakiwa katika kesi hii? Jibu ni kwamba hatuna majina hayo ya washtakiwa na leo hii hawapo kizimbani.
“Maelezo yanataka kuonyesha Sharifu alikuwa akimtembelea Chussa gerezani Babati na huko ndiko mipango ya mauaji ya marehemu Erasto Msuya ilipangwa. Anayakana haya yote.
“Swali la kujiuliza ni je kuna shahidi yeyote kutoka gereza la Babati aliyetoa ushahidi akisema kuna wakati wowote Sharifu aliwahi kufika gerezani na kuongea na Chussa? Hakuna ushahidi huo,” alieleza Magafu.
Wakili huyo aliendelea kudai kuwa wala hakujawahi kuletwa kitabu cha wageni (register book) kuthibitisha Sharifu aliwahi kumtembelea Chussa gerezani wala hakuna shahidi aliyetoa ushahidi huo.
“Hakuna ushahidi huru unaounga mkono yaliyomo katika kile kinachodaiwa kuwa ni confession statement (maelezo ya onyo ya kukiri kosa) ya mshtakiwa wa kwanza (Sharifu Mohamed)” alidai.
Magafu alidai maelezo hayo ni ya uongo kwa vile hata katika utetezi wake, mshtakiwa amekana kumfahamu mshtakiwa yeyote, wala kununua pikipiki wala bunduki iliyotumika.
Ushahidi wa mashtaka, unadai Sharifu ndiye aliyenunua pikipiki mbili, King Lion namba T751 CKB na Toyo namba 316 CLG na bunduki aina ya SMG, vilivyotumika katika mauaji hayo.
“Amekana kwa namna yoyote kuhusika na tukio hili na amekana hajawahi kutoa fedha kwa ajili ya kununua pikipiki na upatikanaji wa bunduki na amekana kuwa na uhusiano wa karibu na Chussa,” aliiambia Mahakama.
Akizungumzia ushahidi wa jumla wa upande wa mashtaka, Magafu alidai hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa aliyewaona wauaji (direct evidence), hivyo wamebakia na ushahidi wa mazingira. “Ili ushahidi wa mazingira uweze kutumika na kuwatia hatiani washtakiwa, mnyororo hautakiwi kukatika na ushahidi unapaswa kuwa madhubuti. Ushahidi wa mashtaka umeacha mapengo mengi.”
Alitolea mfano wa tarehe za kukamatwa kwa washtakiwa na kupatikana kwa bunduki inayodaiwa kutumika katika mauaji hayo, ambazo zinatofautiana kutoka shahidi mmoja hadi mwingine.
Wakili huyo alidai wakati shahidi wa 27 wa mashtaka, Inspekta Damian Chilumba akidai alimkamata Sharifu Agosti 12, 2013 alfajiri, shahidi wa tisa, Inspekta Samwel Maimu alidai alikamatwa Agosti 13, 2013.
“Tunajiuliza hili la tarehe lilitokea bahati mbaya? Tunasema hapana, huu ushahidi ulipikwa. Hawa ni maofisa waandamizi wa polisi kama hilo jambo lingekuwapo wasingejichanganya kiasi hicho,” alidai.
Magafu alidai kuwa wakati shahidi wa 17, mrakibu wa Polisi (SP), Vincent Lyimo akieleza bunduki ya SMG ilikamatwa Septemba 11, 2013, Chilumba anadai ilipatikana Agosti 14, 2013.
Bunduki hiyo yenye namba 1952 KJ 10520 na pikipiki King Lion, zilikamatwa baada ya kukamatwa kwa mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa na mshtakiwa wa sita, Sadik Jabir huko Tabora.
“Ushahidi uliopo katika kumbukumbu za mahakama unaonyesha baada ya kukamatwa Karim na Sadick ndiyo waliwaambia polisi mahali walipoficha bunduki na ilipo hiyo King Lion,” alidai.
“Swali la kujiuliza ni lini Karim na Jabir walikamatwa huko Kaliua? Walikamatwa tarehe 13/9/2013. Sasa unajiuliza pikipiki hii na bunduki ilikuaje zikakamatwa kabla washtakiwa hawajakamatwa?
“Contradiction (kutofautiana) zinazojitokeza, kusigana na kutofautiana kwa ushahidi wa upatikanaji wa pikipiki na bunduki kunakwenda kwenye mzizi wa kesi. Tumwamini nani?” Alihoji Magafu.
Aliendelea kuwa upelelezi wa tukio hilo la mauaji ulianzia katika simu ya marehemu iliyopatikana eneo la tukio na ilionekana simu namba 0682 405 323 iliwasiliana na marehemu siku moja kabla ya tukio.
“Walianza kutafuta mmiliki wa namba 0682 405 323 ni nani wakakuta imesajiliwa kwa jina la Motii Mongululu. Tumebaki na kitendawili Motii Mongululu ni mshtakiwa. Jibu ni hapana.
“Hii namba inaonyesha iliwasiliana na marehemu tarehe 6/8/2013 na 7/8/2013 (siku ya mauaji). Upande wa mashtaka wameshindwa kuthibitisha ni nani alikuwa akiitumia hii simu,” alidai Magafu.
Mbali na hoja hiyo, Magafu alidai washtakiwa wote wamejitetea kuwa hawakuwapo eneo la tukio na upande wa mashtaka haujaweza kuleta shahidi aliyesema aliwaona eneo la tukio.
“Hakuna ubishi kuwa ushahidi pekee wa aliyeshuhudia tukio hili alikuwa ni kijana wa kimasai, Noel Thomas mwenye umri wa miaka 19 aliyekuwa akichunga ng’ombe. Alikuja hapa hakutambua mtu,” alidai Magafu.
Magafu alidai maelezo yote yanayodaiwa kukiri kosa ya Sharifu, mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu, Karim na mshtakiwa wa saba, Ally Majeshi hayakutolewa kwa hiari bali waliteswa. “Ni jukumu la upande wa mashtaka kuthibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa pasipo kuacha mashtaka yoyote na si jukumu la washtakiwa kujinasua na mashtaka dhidi yao,” alidai Magafu.
 Majumuisho ya Jamhuri
Hata hivyo, akiwasilisha majumuisho ya upande wa mashtaka, Chavulla alieleza kuwa wameweza kuthibitisha shtaka pasipo kuacha shaka na kwamba washtakiwa wote walishiriki mauaji hayo.
“Ni maoni yetu kwamba, kwa ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi wetu ni kwamba si wengine walihusika kumuua Erasto Msuya bali washtakiwa waliopo mbele yako,” alidai Chavula.
Chavulla anayesaidiana na Omary Kibwana, Kassim Nassir na Ignas Mwinuka aliongeza kuwa: “Washtakiwa wote walihusika kupanga mauaji ya Erasto Msuya na wote walifika eneo la tukio”.
Alieleza kuwa ingawa washtakiwa wote walijitetea siku ya tukio hawakuwapo eneo la tukio, lakini walishindwa kueleza walikuwa wakifanya nini ambacho kiliwazuia kufika katika eneo la tukio.
“Maeneo waliyoyataja kuwa walikuwapo siku hiyo ya tukio inaonyesha kuwa wanaweza kutoka na kuja hadi eneo ambalo mauaji yalifanyikia kisha kurudi walikokuwa,” alisisitiza Chavulla.
Pia, alidai washtakiwa wameshindwa kuleta mashahidi ambao wangeeleza siku ya tukio huko walikokuwa, washtakiwa walikuwa wanafanya nini ambacho kingewazuia kufika eneo la tukio.
“Tulitegemea kwa mazingira ambayo washtakiwa walieleza walikuwapo, wangewaleta mashahidi ambao wangeieleza mahakama kweli washtakiwa walikuwapo maeneo waliyoeleza na siku ya tukio.
“Lakini hakuna aliyeleta shahidi isipokuwa mshtakiwa wa kwanza ambaye alileta mashahidi wawili ambao nao walishindwa kuieleza mahakama siku ya tukio alikuwa wapi na alikuwa akifanya nini,” alidai.
Ushahidi kutofautiana
Akizungumzia suala la ushahidi kutofautiana, Chavula alidai kutofautiana kwa tarehe ya kukamatwa kwa washtakiwa ni jambo la kawaida hasa ikizingatiwa na muda wa kesi hiyo.
“Dosari ndogondogo zilizojitokeza hasa tarehe ni jambo la kawaida kutokana na muda, kwani toka 2013 hadi sasa ni miaka mitano, na kupoteza kumbukumbu ni kawaida kwenye shauri la muda mrefu,” alidai.
Chavulla aliiomba mahakama izingatie ushahidi wote kwa ujumla wake bila kuangalia ukinzani wa tarehe na kusisitiza kuwa ushahidi wa mashahidi wa mashtaka umethibitisha shtaka hilo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Jumatano wakati wazee washauri wa mahakama watakapotoa majumuisho yao ya mwisho ya kile walichokiona katika ushahidi wote wa pande zote mbili.

Comments