Magufuli, Lowassa wamwaga sera
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli akiweka shada la maua kwenye kaburi la hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere huko Butima, Mara jana. Picha ya CCM
Iringa/Ruvuma/Gairo/Bunda.Wakati mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa akikanusha kuwa hana mashamba kama inavyodaiwa, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amesema alikuwa akipokea amri na kutekeleza majukumu, sasa anataka apewe nchi aweze kutoa amri kwa wengine.
Lowassa anayegombea chini ya mwamvuli wa Ukawa unaoshirikisha vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye mji mdogo wa Kibaigwa mkoani Dodoma, alikanusha kumiliki shamba la Lutangos lililopo katika mpaka wa wilaya za Kiteto (Manyara) na Kongwa (Dodoma). “Nawahakikishieni sina ardhi huko na mimi si mwendawazimu na huyo anayesambaza uongo huo akachukue eneo hilo liwe lake,” alisema Lowassa wakati akijibu tuhuma anazodai kutupiwa na wabaya wake.
Lowassa aliyezungumza kwa dakika 15, alisema ni ajabu kwa watu kudhani mtu akiwa maskini ndiye anakuwa kiongozi bora.
“Umaskini siyo uongozi na wanaosema hivyo ni waongo, hakuna mtu anayependa umaskini duniani na nikienda Ikulu nitawaonyesha Watanzania kuwa naweza kuwakomboa. Tutaanza na elimu bure kwa sababu mtoto akisoma ndiyo kila kitu. CCM ni mahodari wa propaganda na sasa wasiwadanganye,” alisema.
Akihutubia mkutano huo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alimshukia mbunge wa jimbo hilo aliyemaliza muda wake, Ahmed Shabiby (CCM), kwa kitendo chake cha kugawa viberiti vyenye nembo za CCM na picha yake, akisema ni kinyume na maadili ya uchaguzi.
Kuhusu ufisadi, Sumaye alisema ni ajabu meno ya tembo kutoka Tanzania kukamatwa China katika makontena na kuhoji nani aliyesafirisha meno hayo?
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema matatizo yanayolikumba taifa kwa sasa yanatokana na nchi kuwa na katiba mbovu, ambayo imempa Rais mamlaka makubwa ya kuamua kila jambo analotaka.
Kampeni za CCM
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Nyamuswa wilayani Butiama, Dk Magufuli aliwataka Watanzania kumchagua kushika nafasi hiyo, akisema atayatimiza yote anayoyaahidi.
“Kwa nafasi ya uwaziri, nalazimika kuomba kibali kwa Rais pale nilipohitaji kutekeleza miradi ya maendeleo, lakini kama nikiwa Rais nitakuwa namaliza…nimetekeleza mengi kwenye uwaziri wangu chini ya Rais Jakaya Kikwete, siwezi kushindwa haya,” alisema Dk Magufuli.
Akihutubia mkutano huo, Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba, alishangaa uamuzi wa mawaziri wakuu wenzake wa zamani, Sumaye na Lowassa kuhama CCM na kuiponda kuwa haijaleta maendeleo tangu uhuru.
Akihutubia katika mkutano wa kumnadi Dk Magufuli, Jaji Warioba alisema kuna kila dalili viongozi hao hawakuujua wajibu wao kipindi walipokuwa wakiitumikia Serikali na kwamba madaraka yao yalikuwa ni kuwashauri marais.
Akionyesha msisitizo, alisema umefika wakati kwa baadhi ya watu wanaotumia jina la Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere kama dira, kujitafakari kwanza kabla ya kumtumia katika kampeni zao.
“Wengine katika kampeni zao wanatumia maneno ya Mwalimu kama wamechanganyikiwa. Huwezi kumtumia Mwalimu kama dira halafu unasema CCM haijafanya kitu, aliijenga Tanzania kwenye misingi na wote waliomfuata wanapita kwenye misingi yake,” alisema Jaji Warioba.
Wasira na Makongoro
Mgombea ubunge jimbo la Bunda kupitia CCM, Stephen Wasira amemvaa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwa anaandaa mazingira ya kufanya fujo, kutokana na kauli zake za hofu kwamba wataibiwa kura siku ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25.
Wasira aliwaambia wakazi wa Nyamuswa wilayani Butiama kuwa Mbowe na chama chake, hawana uwezo wa kushinda uchaguzi, ila kwa kuwa wamegundua udhaifu huo wameanza kuwandaa Watanzania waone fujo ni haki yao baada ya kushindwa.
“Achunge kura zake, tunajua ni kidogo sana na atashindwa, achunge vizuri ili ije kuwa historia kwa kushindwa na mgombea wa kuazima kutoka CCM, “ alisema Wasira.
Mbali na Wasira, Mjumbe wa Kamati ya kumnadi Dk Magufuli, Makongoro Nyerere alimtaka Mbowe kama ana wasiwasi wa kuibiwa kura, awe anahudhuria mikutano ya CCM aone mafuriko ya wapigakura.
Samia Suluhu
Akiwa mkoani Ruvuma, mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alisema Serikali ya awamu ya tano itakomesha ulanguzi wa mazao ya wakulima mkoani humo, kwa kuanzisha viwanda vidogo kila kata kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao yao ya mahindi na kahawa.
Alitoa ahadi hiyo katika mikutano tofauti ya kampeni aliyoifanya katika vijiji vya Kingerikiti na Tingi Wilaya ya Nyasa na Kijiji cha Maguu, wilayani Mbinga.
Samia alisema Serikali ya awamu ya tano itakapoingia madarakani, itajenga viwanda vidogo vitakavyobangua na kusaga kahawa kwa ajili ya kupeleka Mbinga.
“Kuna taarifa kuwa walanguzi wanakuja, Serikali hatujaweza kununua mahindi yote mnayovuna, lakini kuna walanguzi wananunua mahindi yenu kwa bei ya chini, tutakachokifanya ni kuweka viwanda hivyo ili muweze kuuza unga badala ya mahindi.
‘’Lakini pia, tutawekeza katika viwanda vya kuongeza thamani katika mahindi, kusaga mahindi, kufunga na kuuza unga na mtapata pesa nyingi zaidi kuliko mnavyouza sasa hivi,” alisema.
Juma Duni Haji
Kwa upande wake, mgombea mwenza wa Chadema, Juma Duni Haji aliwataka wakazi wa Kijiji cha Kimande mkoani Iringa, kuondoa woga katika uamuzi na kumpigia kura Lowassa ili kunusuru taifa katika mfumo wa kifisadi.
“Pili, mkituchagua tutafanya yote tuliyoahidi, mfano angalia Magufuli ambaye anajisifu wizara yake inadaiwa Sh1.4trilioni, fedha hizo ukizipanga zinatoka Dodoma hadi Dar es Salaam, kati ya hizo Sh900 bilioni ni adhabu kwa kuchelewesha deni la makandarasi,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Zanzibar), Said Issa Mohamed alisema kila mwaka. Serikali imekuwa ikitenga Sh168 milioni za mfuko wa jimbo, lakini hadi leo hakuna maendeleo ya Isimani. “Zidisha fedha hizo mara miaka 20, aliyokaa bungeni, ni fedha nyingi sana,” aliongeza.
Alisema udhaifu wa Serikali katika kufuatilia fedha za maendeleo ya jimbo, umelifanya Jimbo la Ismani kuendelea kuwa maskini.
“Badala ya kuangalia maendeleo yenu, mnakubali kupokea fulana za CCM bila bukta, ili mtembee uchi siyo... nawaombeni sana msifanye makosa mwaka huu,” alisema Issa.
Mgombea ubunge wa jimbo hilo, Patrick Ole Sosopi alisema ahadi namba nne ni kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, lakini hadi leo wananchi wameendelea kuteseka.

Comments
Post a Comment