Huyu ndiye Dk Bashiru mpenda mijadala, hoja
Kwa wafuatiliaji wa habari na matukio, wanaweza kumfahamu katibu mkuu mpya wa CCM, Dk Bashiru Ally kama mmoja wa wachambuzi maridadi katika hoja mbalimbali za kitaifa.
Naam, ndivyo watakavyokuelezea wanafunzi wenzake wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), walimu wake na wahadhiri wenzake ambao anaachana nao wakati huu akienda kutekeleza masuala ya kiutendaji katika nafasi yake mpya ya katibu mkuu wa chama tawala.
Kwa wasiofuatilia mambo hayo, si rahisi kumjua Dk Bashiru kwa kuwa alikuwa mpenzi wa siasa lakini si mwanasiasa wa kupanda majukwaani kuhubiri itikadi yake, kubishana hoja na anaotofautiana nao au kutetea misimamo ya chama chake.
Bali alishiriki katika mijadala inayotoa fursa kwa mchangiaji kujenga hoja kistaarabu na katika mazingira rafiki, akijaribu kushawishi wale anaotofautiana nao waone kuna haja ya kukubaliana na kile anachokisimamia.
Na hata UDSM iliona uwezo wake katika kuchambua masuala mbalimbali ya kitaifa na ndio maana mwaka 2016 ikamteua kuongoza Idara ya Mijadala na Makongamano yanayoandaliwa na chuo hicho.
Msomi huyo aliyejikita katika sayansi ya siasa na uongozi wa umma, sasa amerithi nafasi iliyoachwa wazi na Abdulrahman Kinana, kanali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambaye naye alipokea kijiti hicho kutoka kwa luteni mwingine mstaafu, Yusuf Makamba.
Tofauti na utaratibu wa muda mrefu wa CCM wa kuteua viongozi wake waliopikwa katika jumuiya zake, Dk Bashiru hakupitia mkondo huo, badala yake ametumia muda mrefu kama mwalimu huku pia akiwa mchambuzi huru wa masuala ya siasa kwenye vyombo vya habari na makongamano ya siasa.
Katika uchambuzi zake, hakusita kuinyooshea kidole CCM au chama chochote pale alipoona kinakwenda kinyume na misingi inayokubalika kisiasa hasa masuala ya ufisadi.
Michango yake katika masuala mbalimbali kama ukuzaji demokrasia na kilio cha Katiba mpya, ndiyo inayoweza kumuweka katika hali ngumu katika kipindi hiki cha mwanzoni mwa majukumu yake mapya.
Kama ilivyokuwa kwa Humphrey Polepole, katibu wa itikadi wa CCM, Dk Bashiru atakabiliana na hali ya kuenea kwa video zilizorekodiwa wakati akifanya mahojiano na vyombo vya habari au kuchangia hoja, zinazoonyesha misimamo yake halisi kuhusu suala la demokrasia na Katiba mpya.
“Tunazungumza mjadala wa Katiba kwa sababu tuna historia ambayo medali ya kujenga muafaka wa kitaifa ilikuwa chama kimoja,”
“Na wakati mwingine unaweza kusema Azimio la Arusha na maazimio mengine ya chama na Muungano, ambavyo vyote ukiangalia vinajidhihirisha katika Katiba hii ya mwaka 1977.
“Tumefanikiwa mengi kujenga Taifa, kujenga umoja wa kitaifa mpaka hapa tulipo. Sisi wasomi wa zao la muafaka wa kitaifa uliojengwa katika zama hizo za chama kimoja, Azimio la Arusha.”
Katika mazungumzo hayo, Dk Bashiru alisema katika miaka ya 1990, nchi iliingia katika mazingira mapya ya kisiasa, mahususi ya kuwa na mfumo wa vyama vingi.
“Kwa hiyo kwa kweli, Katiba hii haiwezi tena ikawa medani ya muafaka wa kitaifa kwa sababu ilisimamia misingi na muafaka wa kitaifa katika chama kimoja,” alisema.
Alisema nchi imekaa kwenye mfumo wa vyama vingi bila mwafaka wa kitaifa.
Alisema ndio maana tangu mwaka 1992, wanasiasa wamekuwa wakidai Katiba mpya kwa kuwa mazingira ni mapya na hivyo ni lazima muafaka ujijenge kutokana na Katiba mpya.
“Kwamba tuko katika mazingira mapya ya kisiasa, mahitaji mapya ya kisiasa, tuna hatua mpya, matarajio mapya, changamoto mpya, taratibu mpya za kuendesha nchi,” alisema.
“Hiyo hoja haitakufa mpaka tumepata Katiba mpya.”
Alishangaa sababu za kutotekelezwa kwa suala hilo licha ya Tume ya Jaji Francis Nyalali kuelekeza njia ya kupata Katiba mpya, akituhumu wanasiasa kuweka masilahi mbele.
Lakini msimamo huo ni tofauti na msimamo wa mwenyekiti wake, Rais John Magufuli ambaye ameshaeleza bayana kuwa Katiba mpya si kipaumbele chake.
Msimamo kama huo alikuwa nao Polepole, ambaye pia alikuwemo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba na kupingana na jinsi Bunge la Katiba lilivyoendeshwa, akikituhumu chama hicho kupuuza maoni ya wananchi yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Katiba. Lakini hivi sasa, katibu huyo wa uenezi wa CCM anazungumzia ukatiba na si Katiba mpya.
Dk Bashiru hakuanza leo kushiriki katika mijadala au kudai haki. Akiwa chuoni alikuwa ni mmoja wa wazungumzaji wakubwa wakati wa harakati za kudai haki za wanafunzi.
Mara nyingi wanafunzi walipokusanyika kwenye uwanja maarufu wa Revolutionary Square, Bashiru aliomba kuzungumza na alipopewa nafasi alikuwa na ushawishi mkubwa kutokana na hoja zake, kwa mujibu wa wanafunzi waliosoma naye.
Pia alitumia elimu yake kudai haki za wananchi, akiwa na taasisi ya HakiArdhi.
Mali za chama
Kama ilivyokuwa kwa Wilson Mukama, kada mwingine wa CCM aliyeongoza kamati iliyoshauri wanachama kujivua gamba na baadaye kupewa kazi ya kutekeleza mkakati huo kwa nafasi ya katibu mkuu, Dk Bashiru atalazimika kukabiliana na hali hiyo atakapoanza kutekeleza mapendekezo ya kamati aliyoiongoza.
Mukama Aprili, 2011 kabla ya kuteuliwa katibu mkuu wa CCM, alikuwa mwenyekiti wa kamati ya kuhuisha chama. Kamati ya Mukama ilikuwa na jukumu la kukitathmini chama ili kiende na hali ya sasa.
Mukama aliongoza kamati iliyofanya kazi kuanzia 2010 hadi 2011 na kuja na mikakati ya kukifanya chama kiendeshwe kisasa na ndipo ukawa mwanzo wa kauli ya CCM kujivua gamba. Pia, Mukama alijitokeza sana kwenye mijadala mbalimbali ya kwenye runinga iliyohusu mwenendo wa siasa nchini, kama ilivyo kwa Dk Bashiru, ambaye mara nyingi hurejea kauli za Baba wa Taifa, Julius Nyerere na ni mmoja wa waandaaji wa Kigoda cha Mwalimu.
Mwalimu Nyerere alimuamini Mukama kiasi cha kumpa nafasi ya mkuu wa Chuo cha Siasa cha Kivukoni. Kwa maneno mengine, alikuwa mkufunzi wa masuala ya siasa kwa wana-CCM ambao wameshikilia madaraka makubwa kwenye chama na Serikali. Hivyo, baadhi ya njia alizopitia Dk Bashiru hadi kuteuliwa kuwa katibu mkuu wa CCM zinafanana kwa kiasi fulani na zile za Mukama.
Kamati ya Dk Bashiru, iliyofanya kazi kwa miezi mitano, ilihakiki mali za CCM ambazo ni pamoja na majengo ya vitega uchumi, hoteli, makusanyo ya maegesho, viwanja vya michezo, vyombo vya habari na mashamba na ilikabidhi ripoti yake kwa mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli.
Habari zinasema ripoti hiyo imewatuhumu vigogo wa CCM, jumuiya zake, mikoa, wilaya na kata kutokana na usimamizi mbovu wa mali hizo, mikataba mibovu, uuzwaji kiholela wa mali na ubadhirifu.
Kamati hiyo iliundwa na Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana Dodoma Desemba 20, 2017. Wajumbe wengine walikuwa ni Walter Msigwa, Albert Msando, Galala Wabanhu, Albert Chalamila, William Sarakikya, Komanya Kitwara, Dk Fenela Mkangara na Mariam Mungula.
Sasa, Dk Bashiru atatakiwa kuwa thabiti katika kushughulikia wakosefu waliotajwa kwenye ripoti yao, jambo ambalo linaweza kuibua mjadala wa uhalali wa kupewa jukumu la kufanyia kazi ripoti ambayo imetokana na uchunguzi wa kamati aliyoiongoza.
Kutetea Azimio la Arusha
Dk Bashiru amekuwa mtetezi wa Azimio la Arusha ambalo ndani yake kuna sera ya Ujamaa na Kujitegemea, huku pia akipinga ukandamizwaji wa kidola na kibepari unaofanywa na Serikali mbalimbali duniani.
Kutokana na utetezi huo, Dk Bashiru anaona suluhisho ni kupata Katiba mpya itakayowapa nguvu wananchi wanyonge.
Akizungumza na gazeti moja la Kiswahili nchini, Dk Bashiru aliwashauri wanasiasa kutowagombanisha wananchi na vyombo vya dola kwa sababu vimeundwa kwa ajili yao.
“Serikali kupitia vyombo hivyo, inapaswa isidhoofishe mchakato wa rasimu ya upatikanaji wa Katiba mpya kwa sababu mchakato huo unapaswa kuwa wa maridhiano, lakini badala yake umekuwa ushirikishwaji wa upande mmoja,” alisema.
Dk Bashiru ni mzaliwa wa Kagera na alipata elimu yake ya msingi na sekondari wilayani Kilosa, kabla ya kujiunga na shule maarufu ya Ihungo kupata elimu ya juu ya sekondari.
Bashiru alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1997, ambako alisomea shahada ya sayansi ya jamii na uongozi wa umma, masomo ambayo alibobea na kubakizwa chuoni hapo hadi akaanza kufundisha na kupewa kusimamia idara ya Makongamano na Mijadala.
Atasimamia mali mwenyewe
Uteuzi wake umepokewa kwa hisia tofauti na wanasiasa na wadau wengine. Spika wa zamani wa Bunge, Pius Msekwa alimpongeza Dk Bashiru Ally kwa uteuzi huo na kusema kuwa ni mtu aliyeonyesha kuwa na uchungu na mali za CCM.
“Sasa hivi atasimamia mwenyewe mali za chama hiki. Wale wote waliobainika katika ripoti yake anawajua baada ya kufanya uhakiki wa mali za CCM,” alisema Msekwa.
“Nimefurahia uteuzi wake. Amepewa madaraka ya kusimamia mali za chama na uendeshaji. CCM itakuwa katika hali nzuri.”
Maalim Seif anena
Pongezi kwa Dk Bashiru pia zilitolewa na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alisema matumaini ya chama chake ni kumuona akiitumia vyema nafasi hiyo.
“Utaitumia vyema kwa kuishauri Serikali na viongozi wenzako ndani ya CCM kuona umuhimu na ulazima wa kurejesha na kuijenga upya Tanzania kwenye misingi ya demokrasia,” alisema Maalim Seif.
Alisema ni muhimu kwa haki za binadamu kuheshimiwa na kuzingatiwa kwa utawala wa sheria.
Alisema ni wajibu wa kila kiongozi kuweka na kutanguliza masilahi mapana ya Taifa kwa kusimamia uadilifu, haki na kuweka mbele uzalendo na kwamba lazima masilahi ya Taifa yawe juu ya mipaka ya vyama vya siasa.
“CUF inakutakia utumishi mwema katika majukumu yako mapya. Pia, tunamtakia kila heri na mapumziko mema Komredi Kinana, kutokana na uamuzi wake wa kustaafu utumishi wa medani ya siasa,” alisema Maalim Seif ambaye aliahidi kumuandikia barua ya pongezi jana alasiri.
Juju Danda
Naye katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Juju Danda alimkaribisha Dk Bashiru, akisema ameingia wakati huu ambao hali ya kisiasa imebadilika kuanzia ndani CCM hadi nje.
“Najua ni kiongozi mzuri. Tutaujua uhodari wake zaidi kwa sababu ameshaingia kwenye ulingo huu ambao upo tofauti na kazi aliyokuwa akiifanya,” alisema.
“Ingawa uongozi na usomi unakwenda pamoja, atambue kuwa kuongoza taasisi za kisiasa ni kazi ngumu.”
Kuhusu Kinana, Danda alisema ni kiongozi mzoefu, msikivu, makini na amefanya siasa kwa muda mrefu akisaidia kuiweka sawa CCM wakati ilipokumbwa na kashfa mbalimbali ikiwamo ya Escrow.
Danda alisema Kinana ni kiongozi wa asili, kwa sababu alijua kuendesha vikao, kuandika na anapaswa kuigwa kutokana na uwezo wake mkubwa aliojaliwa.
Comments
Post a Comment