Samia ataka matokeo fedha za mikopo kwa vijana
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa halmashauri nchini kufuatilia na kujua matokeo ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya mkopo kwa vijana na wanawake.
Samia amesema hayo leo Februari 11,2018 alipozungumza na wananchi katika Kata ya Mgololo mkoani Iringa.
Amesema halmashauri mkoani Iringa zimetenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa vijana na wanawake.
Mbali ya kutenga fedha hizo, amesema ni muhimu kwa uongozi wa halmashauri hizo kufuatilia kuona mikopo inayotolewa imetatua changamoto zipi.
"Niwapongeze kwa kutenga na kutoa mikopo kwa vijana na akinamama, jambo linalotakiwa kufanya sasa ni kufuatilia kujua mikopo hiyo imejibu changamoto gani?" amesema.
Makamu wa Rais amesema lengo la Serikali ni kuona mikopo inakuwa na tija kwa wananchi na Taifa kwa jumla.
Samia yupo ziarani mkoani Iringa ambako amekagua miradi ya maendeleo na kufanya mkutano ya hadhara.

Comments
Post a Comment