Kampeni kunoga zaidi wiki ya lala salama

Wiki hii wakazi wa majimbo ya Siha na Kinondoni na kata 10 za Tanzania Bara watashuhudia kampeni za motomoto pale vigogo wa vyama vinavyochuana watakapojimwaga katika maeneo yao kutafuta kura katika majimbo mawili ya uchaguzi na kata 10 za Tanzania bara.
Uchaguzi huo unafanyika Jumamosi Februari 17 katika majimbo ya Kinondoni na Siha na kata hizo baada ya waliokuwa wabunge na madiwani ama kujivua uanachama na kukosa sifa za kuendelea kuwa wabunge au sababu nyinginezo.
Uchaguzi huo unaoshirikisha vyama 12 tofauti katika Jimbo la Kinondoni, miongoni mwake vinne vinachuana pia katika jimbo la Siha, unatarajiwa kuwa na mpambano mkali baina ya CCM na Chadema.
Chadema ambayo awali ilikuwa imesusia uchaguzi kutokana na kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi mdogo uliotangulia katika kata 43, safari hii imerejea ikiwa inaungwa mkono na vyama vya NLD, NCCR-Mageuzi, Chaumma na CUF upande wa Katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, licha ya upande wa pili cha hicho chini ya mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba kuwa na mgombea wake.
Vyama 12 vinavyochuana katika uchaguzi huo ni CCM, TLP, SAU, Demokrasia Makini, UMD, DP, CUF, Chadema, NRA, CCK, AFP na Ada – Tadea.
Kampeni za uchaguzi katika majimbo hayo mawili mbali na hoja za kawaida kisiasa na za maendeleo ya maeneo husika, zimebebwa na suala la kujiuzulu kwa waliokuwa wabunge wake, Maulid Mtulia (CUF-Kinondoni) na Dk Godwin Mollel wa Chadema-Siha ambao walivihama vyama vyao na kutimkia CCM.
Kilichokuwa kinajadiliwa zaidi ni hatua ya CCM kuwasimamisha tena walewale waliokuwa wabunge, hoja ikiwa ni kwa nini waombe nafasi yaliyoamua kuiacha wenyewe na kujibiwa na chama tawala kwa kutumia hoja zilizotumika wakati wa kujizulu, kwamba wakiwa CCM ndipo watafanikisha lengo lao la kuleta maendeleo.
Wakati kampeni hizo zikitarajiwa kumalizika Ijumaa mpambano mkali wa dakika za lala salama umeanza kuonekana majimbo, kwa viongozi wakubwa katika vyama mbalimbali kuanza kujitokeza kuzipa pengo la kampeni lililokuwapo.
Licha ya kwamba iliwalazimu baadhi ya wabunge kuacha kuhudhuria mkutano wa Bunge uliomalizika jana, wiki hii wabunge wengi zaidi wanatarajiwa kukusanyika kwenye maeneo mbalimbali ya kampeni kujaribu kusaka kura za lala salama.
Kampeni za diwani zafufuka
Katika chaguzi za awali, kama ule wa kata 43, vyama vilikuwa vikichuana vikali tangu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipopuliza kipenga kuashiria kuanza kwa kampeni, safari hii hali imekuwa tofauti. Wakati kampeni hizo zinaanza wiki mbili zilizopita, zile za madiwani zilikuwa zinasuasua na viongozi wengi wa kitaifa walionekana kukamia zaidi zile za ubunge. Viongozi wa vyama vya Chadema, CCM, CUF na TLP wamekuwa wakionekana katika majukwaa hayo wakiwanadi wagombea wa nafasi ya ubunge tangu mwanzo baadhi wameanza kuonekana katika kata mbalimbali.
Kwa upande wa CCM waliojitokeza ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Rodrick Mpogoro, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphey Polepole, Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mwigulu Nchemba, mjumbe wa NEC, Stephen Wasira na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM, Gaudensia Kabaka.
Wiki iliyopita chama hicho kilianza kuongeza nguvu kwa kuwaleta wabunge mbalimbali wakiwamo Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde na Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Matha Mlata na aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba.
Pia, viongozi wake wakuu wameanza kujitokeza katika kata mbalimbali akiwamo Mpogoro, Polepole na Mwigulu kuwanadi wagombea wa udiwani wanaopeperusha bendera ya chama hicho.
Kama ilivyo kwa CCM, Chadema nayo imeanza kuwatuma viongozi wake wa juu kuwanadi baadhi ya wagombea wa udiwani baada ya siku za awali kupambana zaidi na majimbo mawili.
Baadhi ya viongozi walioonekana kwenye kampeni hizo, ni Mwenyekiti Freeman Mbowe, mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji, Naibu katibu Mkuu, John Mnyika na Makamu mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mohamed.
Pamoja na mambo mengine, kampeni hizo zimeibuka na matukio mbalimbali kama la mgombea udiwani wa Kata ya Buhangaza wilayani Muleba (Chadema) kutoweka katika mazingira ya kutatanisha na kupatikana akiwa katika hali mbaya, akieleza alikuwa ametekwa.
Matuko mengine ni ya wagombea wa udiwani kwa tiketi ya Chadema kutangaza kujiunga na CCM. Hili lilitokea wilayani Chamwino katika Kata ya Manzase.
Wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema hatua ya vyama hivyo kuamua kupeleka vigogo wao katika kampeni dakika za lala salama utavisaidia kuongezea kura.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudens Mpangala anasema kipindi cha kampeni ndiyo muda mzuri wa kutumia fursa ya kuzungumza ajenda za chama ili zieleweke kwa wapiga kura.
“Ni fursa nzuri. Haijalishi unagombea udiwani au ubunge, vyama vimeliona hili ndiyo maana wakaamua kutumia nafasi hiyo kupeleka hoja kwa wananchi,” anasema.
Ilivyokuwa kata 43
Katika uchaguzi mdogo wa marudio katika kata 43 mwishoni mwa mwaka jana vyama vyote viliamua kutumia vigogo wake na nguvu kubwa kuwanadi wagombea wao.
Kwa upande wa Chadema Mbowe alizunguka karibu nchi nzima katika kata zote zilizokuwa zikifanya uchaguzi huo huku Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na katibu wa zamani wa itikadi na uenezi, Nape Nnauye wakiibukia Arusha kuwanadi wagombea wa chama hicho.
Vyama vyazungumza
Akizungumzia dhana iliyojengeka kuwa kampeni za udiwani katika Jimbo la Siha zimemezwa na zile za ubunge, Katibu wa Chadema mkoa Kilimanjaro, Basil Lema anakiri kuwa hilo liko dhahiri.
“Kampeni zake hazisikiki kwa sababu ni kawaida kampeni za ubunge lazima zitazipiku za chini lakini si kwamba kampeni hazifanyiki,” anasema.
“Sisi Chadema kwenye udiwani tuna ratiba katika kila kata, tuna timu ya kampeni na kuna mameneja wa kampeni katika kila kata na pia kuna ngome watu wanalala hukohuko,” anasisitiza.
“Kinachojitokeza safari hii ni kwamba viongozi wetu wengi wa kitaifa ni wabunge na kama unavyojua Bunge linaendelea kwa hiyo wako huko, lakini kazi inapigwa si mchezo huko kwenye kata,” anaogeza.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa Kilimanjaro, Jonathan Mabhia anasema kuwa ratiba ya kampeni za madiwani ziko kama kawaida na kwamba kampeni zinaendelea kama zinazoendelea za bunge.
“Ratiba huko kwenye kata inaendelea kama kawaida. Wagombea na kampeni timu zao wanaendelea na kampeni zao tatizo linalofanya hazisikiki ni kwamba taarifa zao haziripotiwi magazetini.”
Kwa mujibu wa Mabhia, wagombea hao wa udiwani huungana na mgombea ubunge wakati akiwa katika ratiba ya kata zao na hilo halimaanishi kwamba hawaendelei na kampeni na kwamba moto ni uleule.

Comments