Watuhumiwa kesi za ugaidi wavua nguo mahakamani


Arusha. Baadhi ya mahabusu wanaokabiliwa na tuhuma za ugaidi, jana walizua tafrani katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini hapa baada ya kuvua nguo wakipinga kuchelewa kukamilika kwa upelelezi wa kesi zao.
Waliovua nguo ni kati ya watuhumiwa 61 wanaokabiliwa na tuhuma hizo za ugaidi na ambao wako katika Gereza la Kisongo.
Kabla ya kushuka kutoka kwenye karandinga baada ya kufika mahakamani hapo saa 3:30 asubuhi, baadhi yao walivua nguo na kusababisha utaratibu wa kuwapeleka chumba cha mahabusu kabla ya mahakamani kuingia dosari.
Askari Magereza walilazimika kuimarisha ulinzi mahakamani hapo huku wakiendelea na jitihada za kuwataka wavae nguo zao lakini waligoma na hivyo kulazimika kuwapeleka chumba hicho wakiwa hawajavaa chochote.
Baada ya kuwafikisha mahabusu na kuwaacha huko, askari hao waliwachukua watuhumiwa ambao hawakuwa wamevua nguo na kuwapeleka mahakamani kusikiliza shauri lao.
Pamoja na kufanya kituko hicho kupinga kucheleweshwa kwa upelelezi, hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Patricia Kisinda aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 30 kutokana na upelelezi kutokamilika.
Mara baada ya kuahirisha shauri hilo watuhumiwa hao walirudishwa ndani ya chumba cha mahabusu ambako walikaa humo kwa muda na wenzao waliokuwa wamevua nguo kabla ya kupandishwa  kwenye  karandiga kurejea Kisongo.
Mbali na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi, baadhi yao wanatuhumiwa kutoa msaada wa fedha kufadhili mpango huo.
Watuhumiwa 13 wanadaiwa kufanya mauaji na kujaribu kuua. Wanatuhumiwa kuwa mwaka 2014 waliwaua Judith Mushi, Ramadhan Juma, Fahad Jamal na Amir Daffa katika Uwanja wa Soweto, Arusha.
Wengine 10  wanatuhumiwa kukusanya zana, yakiwamo mabomu na kuzisambaza kati ya Julai 22 na 23, 2015 kwa lengo la kufanya ugaidi.
Wanne wanatuhumiwa kummwagia tindikali Mustapha Kiago kati ya Julai 2009 na Julai 2013 katika eneo la Msikiti Mkuu wa Arusha na kumsababishia majeraha.
Washtakiwa wengine wanne wanatuhumiwa kutupa bomu la kienyeji nyumbani kwa Sheikh Abdulkarim Njonjo kati ya Oktoba Mosi na 25, 2012 na kumsababishia majereha mwilini. Wengine watatu katika kesi hiyo wanatuhumiwa kushawishi vijana kujiunga na kikundi cha ugaidi cha Al-Shabaab, vitendo wanavyodaiwa kuvifanya kati ya Machi 8 na Julai 14, 2014.

Comments

Popular Posts